Story by Gabriel Mwaganjoni-
Waziri wa Elimu Prof George Magoha amewataka wanasiasa kutoingiza siasa katika swala la elimu, akisema sekta hiyo imesimamiwa ipasavyo chini ya uongozi wake.
Akiwahutubia Wanahabari alipozuru shule za upili za Changamwe na Bomu katika eneo bunge la Changamwe kaunti ya Mombasa, Magoha amesema sekta ya elimu imeimarika na amejitolea kuukabili ufisadi miongoni mwa wasimamizi wa sekta hiyo.
Magoha amekariri kwamba katika kipindi cha takriban miezi minane iliyopita, serikali imejenga jumla ya madarasa elfu 10 yatakayowakimu wanafunzi wanaokamilisha masomo yao ya CBC mwaka huu na akaongeza kwamba zaidi ya madawati laki 6 yamesambazwa katika shule hizo.
Hata hivyo ameongeza kwamba japo Wizara ya elimu ilikabiliwa na ufisadi, juhudi zake za kuuzima ufisadi zimefaulu pakubwa huku akisisitiza kwamba Wizara ya elimu imeboreshwa sawa na kuwekwa mazingira bora kwa walimu na wafaunzi.
Wakati uo huo amewataka wanasiasa kukoma kutia dosari Wizara hiyo huku akimtaka Waziri atakayeongoza Wizara hiyo baada ya kukamilisha muhula wake kuendeleza juhudi za kuikuza sekta ya elimu nchini hasa mfumo wa CBC.