Story by Ali Chete-
Waziri wa Elimu nchini Prof George Magoha amewahakikishia watahiniwa wote wa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE mwaka huu kwamba usalama wao umezingatia kikamilifu.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa baada ya kufanya ziara ya kielimu ya kukagua ujenzi wa madarasa ya mtaala wa CBC katika shule ya upili ya wasichana ya Star of the Sea, Waziri Magoha amesema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha maafisa wa usalama wanashika doria katika vituo vyote ya mitihani ya kitaifa.
Waziri Magoha amewatahadharisha wale wanaoeneza propaganda kuhusu mitihani hiyo katika mitandao ya kijamii na kuwahadaa wanafunzi, akihoji kwamba yeyote atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba mtaala mpya wa CBC ni bora zaidi kwani serikali ya kitaifa pamoja na zile za kaunti zinashirikiana kuuboresha huku akisema tayari kaunti nne zikiwemo Meru, Garissa, Mandera na Wajir zimefikisha asilimia 100 ya utekelezaji wa mtaala huo.
Hata hivyo amewataka wazazi kufuatilia kwa karibu mno mienendo ya watoto wao wakati huu ambapo wako majumbani kwa likizo ndefu ili kuwaepusha na visa vya utovu wa nidhamu.