Taarifa na Charo Banda
Malindi, Kenya, Juni 19 – Kama njia moja wapo ya kukabiliana na msongamano wa wafungwa nchini sasa idara ya magereza imeweka wazi kwamba ipo haja ya kupanua magereza ama kuongeza magereza zaidi kutokana na idadi ya wafunga inayongezeka kila uchao.
Akiongea na wanahabari baada ya kutembelea na kukagua Gereza la Mtangani huko Malindi kamishena mkuu wa Magereza nchini Wycliff Ogola amehoji kuwa tayari idara hiyo imetenga fedha ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wafungwa katika magereza humu nchini.
Amesisitiza kuwa gereza la Malindi linakumbwa na msongamano kutokana na kuongezeka kwa idadi ya mahakama katika kanda hiyo, hivyo basi kuchangia pakubwa msongamano wa wafungwa.
Wakati huo huo amepongeza serikali kutokana na mageuzi katika idara ya mahakama akisema kuwa wafungwa sasa wanakila sababu ya kutabasamu kutokana na jinsi wanavyotangamana na maafisa wa gereza na hata kupata fursa ya kutembelewa na familia zao.