Picha kwa Hisani –
Magavana wanaendelea kuwalaumu maseneta kwa kulemaza shughuli katika kaunti za humu nchini kwa kuchukua muda mrefu kukubaliana kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.
Akizungumza na wanahabari gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amesema kufikia sasa baadhi ya wafanyikazi wa serikali za kaunti hawajapokea mishahara ya mwezi Julai na Agosti mtawalia.
Kahiga amesema licha ya baraza la magavana kupitia mwenyekiti wao Wycliff Oparanya kufika mahakama ya juu zaidi kutafuta suluhu juu ya ugavi wa fedha kwa kaunti lalama zao zimepuuzwa.
Haya yanajiri huku baraza la magavana nchini likitishia kuzifunga kaunti zote 47 nchini iwapo maseneta watashindwa kuafikiana kuhusu mfumo huo wa ugavi wa mapato.