Shughuli za matibabu katika hospitali na zahanati zote za umma Kaunti ya Mombasa zitasambaratishwa endapo Serikali ya Kaunti hiyo haitatimizia madaktari matakwa yao.
Madaktari wa Kaunti hiyo wanatarajiwa kutoa ilani ya mgomo wao hii leo ili kuishinikiza serikali ya kaunti ya Mombasa kuwalipa marupuru yao sawia na kuwapandisha vyeo kulingana na makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Katibu mkuu wa Chama cha madaktari tawi la Kaunti ya Mombasa Daktari Abidan Mwachi amesema Madaktari hao licha ya kuhudumu katika mazingira hatari hasa wakati huu wa janga la Corona hawana bima za afya na serikali ya kaunti ya Mombasa haijata tamko lolote kuhusiana na kauli ya madaktari hao.
Kando na hayo ya Mombasa tayari wahudumu wa afya katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta wameanza rasmi mgomo wao hii leo wakiapa kutorejea kazini hadi pale tume ya SRC itakapowaongezea mishahara.