Story by: Rasi Mangale
Waziri wa Elimu nchini Ezekiel Machogu amesema wanafunzi wa mtihani wa kitaifa wa KCSE mwaka wa 2022 wamefanya vyema ikilinganishwa na wale wa mwaka 2021.
Waziri Machogu ameweka wazi kwamba idadi ya wanafunzi waliopata alama ya A ni wanafunzi 1,146 kati ya wanafunzi 881,416 waliofanya mtihani huo wa kitaifa wa KCSE mwaka wa 2022.
Akitangaza matokeo hayo katika makao makuu ya baraza la kitaifa la mitihani nchini KNEC jijini Nairobi, Waziri Machogu amesema wanafunzi watakaojiunga na vyuo vikuu imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita kwani wanafunzi 173,345 wamepata alama ya C+.
Waziri Machogu hata hivyo amesema wanafunzi waliopata alama ya D+ ni 522,588 ambayo ni asilimia 59.14 huku wale waliopata alama ya E wakiwa 30,822 ambayo ni asimilia 3.49.
Wakati uo huo amedokeza kwamba serikali itatumia kima cha shilingi bilioni 18 kusimamia elimu ya CBC katika kipindi cha mwaka wa kifedha wa 2022/2023 kwa wanafunzi wa gredi ya saba na fedha hizo zitasambazwa shuleni ambapo kila mwanafunzi atapata shilingi elfu 15 ambapo shilingi elfu nne zitatumika kuboresha maabara.