Maafisa wawili wa polisi wameripotiwa kufariki huku watu wengine 10 wakijeruhiwa vibaya baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa polisi kaunti ya Kwale , Tom Odero amesema polisi hao wawili walikuwa wameabiri tuktuk iliyogongana ana kwa ana na matatu ya abiria katika eneo la Magandia kwenye barabara ya Likoni -Lungalunga.
Odero amesema tayari uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo huku akiwataka wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma na tuktuk kuwa makini zaidi wanapokuwa barabarani.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo wamekimbizwa katika zahanati ya Waa huku wengine wakikimbizwa katika hospitali ya Kwale kwa matibabu ya dharura.
Miili ya maafisa hao wawili wa polisi inahifadhiwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.
Taarifa na Salim Mwakazi.