Maafisa wa Polisi Mjini Mombasa wamemtia nguvuni mshukiwa mmoja wa ujambazi ambaye amekuwa akiwahangaisha wakaazi katika eneo la Mji wa Kale.
Mshukiwa huyo kwa jina Hassan Noordin Abdallah amenaswa mapema leo akiwa kwenye chumba kimoja katika eneo la Kibokoni huku visu aina ya machete, mapanga na simu kadhaa za rununu vikipatikana.
Afisa mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Augustine Nthumbi amekiri kwamba Abdallah ametiwa nguvuni kufuatia ukanda wa video uliyowaonyesha vijana wawili wakimvamia mtu mmoja katika eneo la Mji wa kale siku moja iliyopita. Nthumbi amesema Abdallah anahojiwa na maafisa wa usalama ili kufichue washirika wake.
Hata hivyo maafisa wa usalama wanaendeleza oparesheni ya kiusalama katika eneo zima la mji wa Kale wakiwasaka washirika hao wa uhalifu.