Taharuki imeshuhudiwa tena katika mji wa Malindi mapema leo baada ya maafisa wa GSU pamoja na maafisa tawala kuendeleza oparesheni kali mjini humo kuwasaka wahudumu wa boda boda waliompiga kamanda wa trafiki eneo hilo.
Oparesheni hiyo ilioongozwa na kamanda wa polisi katika eneo la Malindi imepelekea shughuli za kawaida katika mji wa Malindi kusitishwa wakati wa purukushani hizo zilizochukua zaidi ya masaa matano.
Kamanda wa polisi eneo la Malindi Vitalis Otieno amesema oparesheni hio itaendelezwa hadi pale wahudumu wa boda boda waliompiga na kumjeruhi kamanda wa trafiki eneo la malindi George Naibei wanatakaponaswa.
Hata hivyo wahudumu wa boda boda mjini Malindi wakiongozwa na mwenyekiti wao Joseph Mwangu wamekashifu oparesheni hio wakiwataka maafisa wa polisi kuwasaka waliohusika na uovu huo na wala sio kuhangaisha wakaazi wote wa Malindi.