Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili na mshindi wa Tusker Project Fame season 5, mwaka wa 2012, Ruth Matete amempoteza mumewe John Apewajoye ambaye alikuwa pasta, miezi michache tu baada ya kufunga harusi. Kifo chake kinatokana na majeraha aliyoyapata kufuatia ajali ya mlipuko wa gesi nyumbani kwao.
Kupitia ukurasa wa Facebook wa mwimbaji huyo, Ruth alithibitisha kifo hicho na kuomba mashabiki wake wamsaidie kwa maombi wakati huu mgumu kwake.
Kulingana na ripoti iliyotufikia, marehemu, mchungaji John Apewajoye, alikuwa anajaribu kukarabati mtungi wao wa gesi ambao ulikuwa umekoma kufanya kazi. Alitoa mtungi huo nje na kujaribu kutoa gesi kiasi na kuurudisha katika nyumba na kujaribu kuwasha ambapo ulilipuka.
Dokezo zimedai kwamba, wakati alipokuwa anapunguza gesi, ilifyonzwa na nguo ambazo zilikuwa zimeanikwa kwenye kamba, na alipokuwa anawasha gesi baadaye, nguo hizo zilishika moto na kwa bahati mbaya kumpata. Ruth, kupitia usaidizi wa majirani waliweza kuzima moto huo na mumewe akapelekwa hospitalini ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Inasemekana mwanamziki huyo alikuwa amedokezewa kuwa mumewe hakuwa hatarini na angeendelea kupona pole pole lakini mambo yaligeuka kuwa tofauti alipokata roho na kuaga dunia siku chache baada ya kuondolewa chumba cha wagonjwa mahututi. Wawili hao walikuwa wanatazamia kujaliwa mtoto wao wa kwanza pamoja ambapo Ruth kwa sasa ni mja mzito.
Radio Kaya inaomba Mungu kuzifariji familia za Ruth na mumewe na ailaze roho ya mwendazake mahali pema peponi.