Picha kwa hisani –
Zaidi ya wakaazi 300 wa eneo la Kambini huko Tsunza Gatuzi dogo la Kinango Kaunti ya Kwale wanalilia haki kwa madai ya kupokonywa ardhi yao ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara ya Dongo kundu bila ya kufidiwa.
Wakiongozwa na Saumu Athuman,wakaazi hao wamesema wamekuwa wakifurushwa kwenye ardhi yao yenye hekari 15 na ambayo walipaswa kufidiwa shilingi milioni 52.
Saumu amesema ardhi hiyo ilibadilishwa kisiri kwa mmiliki tofauti huku Wizara ya ardhi katika Kaunti ya Kwale ikihusika pakubwa katika dhuluma hiyo.
Kwa upande wake,Mzee Jumaa Mwinyi amesema dhuluma hiyo imewaweka katika hali ya wasiwasi na kwamba licha ya kuzuru afisi zote ikiwemo ya Mbunge wa Kinango Benjamin tayari hawajasaidika.
Hata hivyo, Maafisa tawala akiwemo Naibu Chifu wa Gandini Munga Ndegwa wamesema hawahusiki na unyakuzi huo wa ardhi,huku wakaazi wakishikilia kwamba Maafisa hao wanahusika mno na kuwanyang’anya ardhi yao.