Takriban wanyama milioni 500 wamekufa katika eneo la New South Wales pekee huko Australia huku mamia ya watu wakiachwa bila makao kufuatia moto mkubwa wa nyika unaoendelea kushuhudiwa.
Msimu wa moto wa nyika huwa ni jambo la kawaida Australia ila mwaka huu moto huo umeripotiwa kuwa mbaya zaidi. Tangu mwezi Septemba watu 19 wameripotiwa kufariki huku zaidi ya 12 wasijulikane waliko. Viwango vya joto vimeripotiwa kufikia nyuzi joto 41. Tayari ekari milioni nne zimeteketea katika moto huo – ekari moja ni sawa na uwanja mmoja wa mpira.
Moto huu ni mgumu kuzimwa kutokana na ukame ukiambatana na upepo mkavu unaosababishwa na hali ijulikanayo kama positive Indian Ocean Dipole.
Hali hii hutokea pale eneo la bahari hindi linalopakana na Pwani ya Afrika mashariki linaposhuhudia joto jingi huku eneo linalopakana na Australia linapokuwa na kiwango cha chini cha joto. Hali hii hupelekea mvua kubwa kunyesha Afrika mashariki huku Australia ikisalia kuwa bila mvua.
Vilevile itakuwa vigumu kuuzima moto huo kwani msimu wa ukame unatarajiwa kuisha mwezi Februari au Machi.
Wanasayansi wamesema kuwa hili ni dhihirisho moja wapo la kuongezeka kwa athari za mabadiliko tabia nchi yaani Climate Change. Ulimwengu kwa sasa upo na viwango vya juu vya joto kutokana na kupungua kwa kiwango cha misitu na uchafuzi wa hewa unaofanywa na viwanda.
Ili kupunguza athari hizi tunashauriwa kupanda miti kwa wingi na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mola awape subra wakati huu mgumu