Picha Kwa Hisani – Oluoma Chimenye John
Kasisi wa kanisa la Katoliki nchini Nigeria, Oluoma Chimenye John, amezua mjadala mitandaoni, baada ya mkanda wa video alioweka kwenye ukurasa wake wa Instagram kusambaa akiwashauri waumini kutumia pombe.
Katika mkanda huo wa video, kasisi huyo anasikika akisema kwamba pombe ni dawa na kuwashauri washirika wake kuitumia kwa sababu kitendo cha kuitumia pombe hakitawazuia hata kidogo kuuona ufalme wa mbingu.
“Hata kama mtakubali au kupinga, pombe inatumika kama dawa. Ikunywe kwa kiwango. Kunywa pombe, kunywa divai. Kila kitu ambacho mungu aliumba, kama pombe hivi ukiitumia kwa kiwango kama inavyostahili, itakufaidi,” kasisi huyo alieleza
Wapenzi wa pombe wamefurika mitandaoni kumlimbikizia sifa kasisi huyo kwa kutakasa pombe huku walokole wakiwa na maoni kinzani kwamba mhubiri huyo anapotosha watu wa Mungu.
Picha Kwa Hisani – Oluoma Chimenye John
Kaisi huyo anasikika akiwaambia waumini kuwa pombe haiwezi kuwa mbaya kwa sababu ni kitu ambacho Mungu aliumba, na chochote ambacho Mungu aliidhinisha ni safi.
“Jivinjari katika divai yenu, kwa wote wote ambao ni wapenzi wa pombe, Mungu asifiwe? Na kwa wale hamtumii mvinyo Mungu asifiwe? Hata kama hutumii kinywaji, tukubalie sisi wale tunatumia pombe tujivinjari. Wote tutakutana mbinguni,” alisema Oluoma Chimenye John.