Kituo maalum cha uvumbuzi kitazinduliwa katika eneo bunge la Mvita ili kuwawezesha vijana kutumia uwezo wao katika kuvumbua huduma na vitu mbalimbali vitakavyowawezesha kubuni ajira na kujikimu kimaisha.
Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir, amehoji kwamba jitihada hizo zitapelekea vijana wengi kukumbatia utafiti na kupitia kwa talanta zao kuvumbua vitu vinavyolenga sio tu kuwawezesha kujiajiri bali pia kuboresha hali ya maisha ya jamii yao.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita hii leo, Nassir amehoji kwamba ni sharti vijana wawezeshwe kuboresha hali yao ya maisha na kutumia elimu na teknolojia katika kubuni ajira akihoji kwamba ulimwengu wa sasa unajiondoa katika maswala ya kutafuta ajira na badala yake kukiwezesha kizazi kichanga kubuni ajira.
Nassir amehoji kwamba hazina mbalimbali za eneo bunge lake zitatumika katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho utakaowanufaisha vijana wote wa kaunti hiyo na wala sio wa kutoka eneo bunge la Mvita pekee.
Amesema tayari mchakato huo umeanzishwa ili kuhakikisha mradi huo unafulu ili kuwanufaisha Vijana.