Story by Gabriel Mwaganjoni-
Kiongozi wa kidini wa jamii ya Shree Swaminarayan Gadi, Swamiji Maharaj amewasili humu nchini kutoka nchini India ili kuongoza maombi maalum kwa taifa hili.
Maharaj atakita kambi katika kaunti ya Mombasa kwa muda wa siku tatu akiliombea taifa ili lizidi kudumisha mshikamano miongoni mwa wananchi wake sawa na viongozi kutekeleza majukumu yao pasipo na ubaguzi wala kuwapendelea na kuwatenga wengine.
Akizungumza kwaNiaba ya Kiongozi huyo, Msemaji wa jamii hiyo nchini Harshad Sanghani amesema Kiongozi huyo mkuu kutoka nchini India atazuru jiji la Nairobi ambako vile vile ataendeleza maombi kwa siku tatu mtawalia, usiku na mchana akiliangazia mno janga la ukame na njaa humu nchini.
Maharaj ambaye amekuwa akizuru Kenya kila mwaka ameweka maombi yake katika vipengele vitatu muhimu vya kukemea ukame, baa la njaa na umaskini, kuombea mvua, kuwaombea viongozi kuyawajibikia majukumu yao sawa na kuombea mshikamano wa nchi, huku kiongozi huyo akifurahishwa mno na uchaguzi wa amani uliyoshudiwa nchini.
Baada ya muda huo wa siku 6, Maharaj atazuru mataifa ya Tanzania na Uganda kabla ya kurudi nchini India.