Story by Charo Banda –
Kamati maalum ya kutatua mizozo ya ardhi katika eneo la Kadzuhoni kule Magarini kaunti ya Kilifi imebuniwa ili kutafuta suluhu la mzozo wa ardhi baina ya wenyeji na bwenyenye anayedai kuwa mmiliki ardhi hiyo.
Gavana wa Kilifi Amason Jefwa Kingi amesema kamati hiyo imebuniwa baada ya wakaazi wa eneo hilo kudai kuwa hawana imani na kamati ya awali ambayo imefeli kutatua swala hilo.
Gavana Kingi amesema kamati hiyo ya watu 15 inatarajiwa kufanya mazungumzo na bwenyenye huyo na kuafikiana maswala kadhaa yatakayohakikisha wakaazi hao wanapata uhalali wa ardhi hiyo yenye ekari 339.
Naye Mbunge wa Magarini Micheal Kingi amesisitiza haja ya kutoingizwa siasa katika swala hilo tata la ardhi huku akimtaka waziri wa ardhi katika kaunti hiyo kuhakikisha kamati hiyo inapata usaidizi ili kuibuka na suluhu la mzozo huo.
Kwa upande wake Waziri wa ardhi katika serikali ya kaunti ya Kilifi Maurine Mwangovya amesema zaidi ya familia elfu tatu katika ardhi hiyo zimeathirika na mzozo huo wa ardhi.