Picha kwa Hisani –
Spika wa bunge la seneti Ken Lusaka ameahirisha kikao kilichokua kikiendelea cha kujadili mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti hadi saa nane unusu hii leo,baada ya maseneta kushinikiza kihairishwe baada ya wenzao watatu kutiwa nguvuni na maafisa wa polisi.
Lusaka ameitaka kamati ya seneti kuhusu usalama kuwasilisha ripoti kamili mchana wa leo kuhusu kutiwa nguvuni kwa watatu hao akiwemo seneta Cleophas Malala wa Kakamega,Christopher Langat wa Bomet na Steve Ltumbesi Lelegwe wa Samburu.
Akitoa hoja yake kuhusu kuhairishwa kikao hicho seneta wa Kilifi Stewart Madzayo amesema visa vya watu kutiwa nguvuni na kupotea katika hali tata vimekithiri na kwamba lazima watatu hao wafikishwe mbele ya bunge hilo ili ithibitishwe kwamba wako salama.
Kwa upande wake seneta wa kaunti ya Makueni Mutula Kilonzo Junior amesema hawatoendelea na kikao hicho huku wenzao wakiwa mikononi mwa maafisa wa polisi akisema hawatoruhusu viongozi wakuu serikalini kuwanyanyasa wananchi.
Naye seneta wa Elygeyo Marakwet Kipuchumba Murkome amekashifu kutiwa nguvuni kwa watatu hao akimtaka inspekta jenerali wa polisi nchini Hilary Mutiambai kutoa maelezo juu ya suala hilo.
Kwa upande wake seneta wa kaunti ya Tana River Golich Juma Wario amesema hawatakubali utendakazi wa bunge la seneti kuingiliwa na idara zengine za serikali.
Chama cha mawakili nchini LSK kupitia rais wake Nelson Havi kimesema kutiwa nguvuni kwa tatau hao ni ishara kamili kwamba idara ya polisi inatumia vibaya mamlaka yake.
Maseneta hao ambao hadi sasa wanazuiliwa na maafisa wa polisi,wamezuilia tangu mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia leo huku wakikatiziwa huduma muhimu katika nyumba zao ikiwemo nguvu za umeme na maji.