Story by Our Correspondents-
Mgombea huru wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 aliyetemwa nje ya kinyang’anyiro hicho na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Reuben Kigame, sasa amejitokeza na kumtaka Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kujiuzulu.
Katika kikao na Wanahabari, Kigame amesema Chebukati amehujumu uhuru wa wananchi katika zoezi la upigaji kura sawa na kuwatelekeza watu wanaoishi na uwezo maalum kupigania nafasi za uongozi nchini.
Kigame amesema ni vyema iwapo kila mmoja atapewa nafasi katika kinyang’anyiro hicho huku akishinikiza zoezi la kuwaidhinisha wale wote waliotuma maombi ya kuwania kiti cha urais lirudiwe kwa kuzingatia haki na usawa.
Mwanasiasa huyo ambaye anaishi na ulemavu, amezidi kumshtumu Chebukati kwa kuidhalilisha jamii ya watu wanaoishi na ulamavu huku akidai kwamba kuna baadhi ya wagombea wa urais walioidhinisha licha ya kukosa shahada ya masomo.
Wakati uo huo amedokeza kwamba ni lazima wakenya waungane na kuwachagua viongozi wenye malengo bora iwapo wanahitaji taifa hili liwe na rekodi nzuri ya maendeleo.