Watetezi wa haki za kibinadamu katika Kaunti ya Lamu wameidhinisha uchunguzi kufuatia tetesi kwamba mwanamke mmoja ameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 katika hospitali kuu ya King Fahad Kisiwani Lamu.
Wakiongozwa na naibu mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika Bi Salma Hemed, watetezi hao wamemtaka waziri wa afya wa kaunti hiyo Daktari Anne Gathoni kuweka bayana kuhusu taarifa hiyo kwani wakaazi wamejawa na hofu.
Kulingana na Bi Hemed kinyume na madai kwamba serikali ya Kaunti hiyo imetenga kituo maalum kilicho na jumla ya vitanda 30 kuwahudumia wagonjwa wa Corona, hospitali hiyo haina hata kitanda kimoja cha kutoa huduma hiyo.
Bi Hemed amesema watetezi wa haki watafanya mkao na gavana wa kaunti ya Lamu Fahim Twaha na Maafisa wakuu wa Idara ya afya ya Kaunti hiyo ili kubaini kuhusu maandalizi ya kukabiliana na virusi vya Corona Kaunti ya Lamu.