Mahakama kuu mjini Mombasa imehairisha kwa mara ya pili kikao cha kutoa uamuzi wa kesi ya rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 10 gerezani alichopewa mjane wa marehemu Sheikh Aboud Rogo, Bi Hanniah Saggar Rogo.
Jaji wa Mahakama hiyo Dora Chepkwony amesema uamuzi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo basi mshtakiwa atalazimika kusuburi gerezani hadi uamuzi wa kesi hiyo utakapokamilika ndipo ajue hatima yake.
Kwenye uamuzi uliyotolewa awali na Jaji wa Mahakama ya Shanzu Diana Mochache, mshtakiwa alipatikana na makosa ya kushindwa kuzuia uvamizi uliotekelezwa katika kituo cha Polisi cha Central mjini Mombasa miaka miwili iliyopita.
Jaji Mochache alisema hukumu iliyotolewa kwa Mjane wa Marehemu Sheikh Aboud Rogo ni pamoja na kupatikana na makosa ya kufanya mawasiliano na washukiwa watatu wa ugaidi waliokishambulia kituo hicho cha polisi mnamo tarehe 11 mwezi Septemba mwaka wa 2016.
Mjane wa Rogo anataka Mahakama hiyo kumuondolea hukumu hiyo ya miaka 10 gerezani, akisema ilitolewa bila ya kuzingatia kanuni na Katiba ya nchini. Mahakama hiyo sasa itatoa uamuzi wake dhidi ya kesi hiyo mnamo tarehe 5 mwezi Oktoba mwaka huu.
Taarifa na Hussein Mdune.