Story by Gabriel Mwaganjoni-
Kesi inayohusu mzozo wa ardhi kati ya zaidi ya familia 3,000 na kampuni tatu tofauti zinazodai umiliki wa ardhi ya ukubwa wa ekari 55 ya Utange katika eneo bunge la Kisauni kaunti ya Mombasa imerudi tena Mahakamani baada ya kusitishwa kwa kipindi cha miaka 6.
Katika kesi hiyo, Wakaazi wanaoishi katika ardhi hiyo Wakiongozwa na Stephen Safari wamekishtaki Chama cha Ushirika cha Bamburi Wananchi Sacco, Khatiby Group of Companies Limited na mwekezaji wa kibinafsi raia wa Bara Asia kwa madai ya umiliki wa ardhi hiyo licha ya kukosa stakabadhi halisi za kuthibitisha umiliki huo.
Mawakili wa maskwota hao waliyovunjiwa nyumba zao wakiongozwa na William Kenga na Omondi Okanga wameiambia Mahakama kwamba chama hicho kiliinyakua ardhi hiyo na stakabadhi wanadai kuwa nazo za kuonyesha kwamba walinunua ardhi hiyo tangu mwaka wa 1982 ni uongo.
Chama cha ushirika cha Bamburi wananchi Sacco kimeiambia mahakama kwamba kilitumia kima cha shilingi milioni 1.8 kununua kipande cha ardhi hiyo iliyo katika eneo la Utange japo usimamizi wake ulipotakiwa kuwasilisha stakabadhi za kuonyesha ununuzi huo ulishindwa kuonyesha stakabadhi hizo na kuzua utata mahakamani.
Kesi hiyo inaendelea huku maskwota hao wakiwasilisha mbele ya Jaji Naikuni matakwa yao ya kutaka hati miliki zote za ardhi zinazomilikiwa na watatu hao kufutiliwa mbali wakishikilia kwamba watatu hao walinyakua ardhi hiyo.