Story by Gabriel Mwaganjoni –
Kesi ya mauaji inayomuandamana Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mlinzi wake Geoffrey Otieno Okuto imeahirishwa katika mahakama ya Mombasa baada ya Mawakili wanne waliyokuwa wakiwawakilisha wawili hao kuiambia mahakama kwamba hawatamwakilisha tena Okuto.
Mawakili hao Jared Magolo, Cliff Ombeta, Danstan Omari na Shadrack Wamboi wamesema wameamrishwa na Jumwa kutomwakilisha Okuto sawa na kuiomba mahakama kuiondoa dhamana ya shilingi nusu milioni ya Okuto.
Wakili Omari amemwambia Jaji wa mahakama kuu Njoki Mwangi kwamba tayari Okuto amefahamishwa kuhusu mabadiliko hayo, akisema kwamba Jumwa amewaamuru mawakili wake kutotoa huduma zozote mahakamani kwa Okuto.
Kwa upande wake, Okuto ameiomba mahakama kumpatia muda zaidi ili atafute wakili sawa na mdhamini tofauti kutokana na kuondolewa kwa mdhamini wake.
Jaji Mwangi ametaka pande zote kuafikiana kuhusu muda unaostahili kwa Okuto kupata wakili na dhamana kabla ya kesi hiyo kuendelea mahakamani
Jumwa na Okuto wanakabiliwa na shtaka la mauaji wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda katika eneo la Malindi mnamo mwezi Oktoba mwaka wa 2019.