Picha kwa hisani –
Rais Uhuru Kenyatta amethibitisha kujitolea kwa Kenya kutekeleza mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga ulimwenguni.
Kwenye hotuba yake rais Kenyatta ametoa wito wa juhudi za pamoja ulimwenguni katika kushughulikia mabadiliko ya hali ya anga, Akisema kwa kushirikiana ulimwengu utaibuka imara zaidi na kupata uwezo wa kustahimili hatari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya anga.
Kiongozi wa nchi amesema wakulima wa barani Afrika sharti wapewe vifaa, habari na usaidizi wa kifedha ili kuwawezesha kutumia mbinu za kudumu za kilimo, kukabilana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza uzalishaji.
Rais ameyasema haya jana jioni katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano wa viongozi kwa njia ya video kuhusu Kongamano la hadhi ya juu la Kukabiliana na Mabadiliko ya hali ya Anga la mwaka wa 2021.
Viongozi kadha wa ulimwengu wakiwemo Mawaziri Wakuu Boris Johnson (Uingereza), Narendra Modi (India), Evelyn Wever-Croes (Aruba) na pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na mtangulizi wake Ban Ki-Moon walihudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Waziri Mkuu Mark Rutte wa The Netherlands.