Story by Our Correspondents –
Serikali imepokea shehena mpya ya dozi ya chanjo ya Corona aina ya Pfizer kutoka taifa la Marekani ili kupiga jeki juhudi za kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini.
Akizungumza na Wanahabari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi baada ya kupokea Shehena hiyo yenye dozi 795,000, Katibu katika Wizara ya Afya nchini Susan Mochache amesema chanjo hiyo itasambazwa kote nchini.
Mochache hata hivyo amewaonya wakenya dhidi ya kuhadaiwa na baadhi ya vituo vya afya ambavyo havijaidhinishwa na Wizara ya Afya nchini kupeyana chanjo ya Corona, akiwataka wakenya kuwa waangalifu na chanjo wanazopewa mashinani.
Naye Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya maswala ya kigeni Ababu Namwamba amewahimiza wakenya kujitokeza kwa wingi ili kupokea chanjo, akisisitiza kwamba chanjo husaidia kupeyana kingi dhidi ya maambukizi.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani humu nchini Eric Kneedler ameahidi juhudi za serikali ya Marekani kuendelea kushirikiana na Kenya katika kupambana na maambukizi ya Corona.