Shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini KEBS limetakiwa kusitisha ushindani kati yake na Idara ya afya katika bandari ya Mombasa kwa lengo la kuhimiza ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa humu nchini kupitia bandari hiyo.
Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amebaini kwamba vitengo hivyo viwili vimekuwa vikishindana huku Shirika hilo la KEBS likionekana kudunisha kitengo hicho cha afya cha bandari ya Mombasa licha ya kuwa na umuhimu katika kubaini ubora wa bidhaa hasa zile za vyakula vinavyoingizwa humu nchini.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Changamwe, Mwinyi amehoji kwamba mvutano huo umepelekea bidhaa kama vile sukari, mahindi na mvinyo kupitishwa katika bandari hiyo pasipo na kukaguliwa hali inayohatarisha afya ya Wakenya pindi wanapozitumia bidhaa hizo nyingi zikiwa bandia.
Mbunge huyo vile vile amekosoa ubaguzi wa kiuchumi unaochangiwa na Serikali kuu kwamba makasha yote yanayoingizwa humu nchini yasafirishwe kupitia barabara ya reli ya kisasa SGR akipendekeza kuwepo na mgao sawa wa kiuchumi kati ya SGR na sekta ya uchukuzi wa malori kupitia barabara ya lami.