Serikali ya kaunti ya Taita taveta sasa imeling’oa bango linaloashiria kuwa eneo la ‘Man eaters’ karibu na Mto Tsavo, ni sehemu ya kaunti ya Makueni, ikidai eneo hilo liko ndani ya kaunti ya Taita taveta.
Akizungumza na wanahabari hapo jana waziri wa ardhi kaunti ya taita taveta Mwandawiro Mghanga amesema wana ushahidi wa kutosha unaoashiria kuwa eneo hilo ni Wadi ya Ngulia na limo ndani ya kaunti hiyo.
Kulingana na Mwandawiro kwa miaka mingi sasa, Serikali ya kaunti hiyo imekuwa ikitoa huduma msingi kwa wakaazi wa eneo hilo na haliwezi kuwa ndani ya kaunti ya Makueni.
Wakati uo huo, Mwandawiro ameshinikiza umuhimu wa mazungumza kati ya Serikali za kaunti hizo mbili kuhusu utata huo wa mipaka ili kuutanzua.