Story by Gabriel Mwaganjoni –
Serikali ya kaunti ya Lamu imehimizwa kuzifidia zaidi ya familia 50 zilizoondolewa kwenye ardhi zao ili kutoa nafasi ya ujenzi wa makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu.
Watetezi wa haki za kibinadamu kaunti ya Lamu wakiongozwa na Shirika la Lamu Justice Network wamesema miaka minane sasa tangu familia hizo zitimuliwe kwenye ardhi zao bado hazijafidiwa.
Akizungumza katika eneo la Mokowe kaunti ya Lamu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Yunus Ahmed amesema licha ya bunge la kaunti ya Lamu kupitisha mswada wa kufidiwa kwa familia hizo bado swala hilo halijatekelezwa.
Wakati uo huo, Ahmed amesema wanaharakati hao watazindua upya mchakato wa kushinikiza fidia kwa waathiriwa hao ambao kwa sasa wanaishi katika hali ya umaskini kwani hawawezi tena kujiendeleza katika maswala ya kilimo.