Story by Mwanaamina Fakii –
Wizara ya Afya katika kaunti ya Kwale imepokea ufadhili wa vifaa 400 vya kudhibiti maambukizi ya Corona kutoka kwa Wakfu wa Aga khan.
Waziri wa Afya katika serikali ya kaunti hiyo Francis Gwama amesema vifaa hivyo vitawasaidia pia wahudumu wa afya katika kutekeleza majukumu yao ya kupambana na maambukizi ya Corona.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kupokea vifaa Gwama amesema vifaa hivyo vinajumuisha pamoja na vile vya kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili kuboresha huduma zao.
Wakati uo huo amedai kwamba vifaa hivyo vitasambazwa katika hospitali zote kaunti ya Kwale na kutumika kwa mujibu wa makubaliano.
Kwa upande wake Afisa mkuu mtendaji wa Hospitali ya Agha Khan Syed Sohali amesema msaada huo utawasaidia wahudumu wa afya kujikinga dhidi ya Corona na vile vile kuwapa ujuzi zaidi.