Kampuni ya usambazaji maji katika kaunti ya Tana river ya TAWASCO imesema itawekeza katika teknolojia ya kisasa ili kuongeza pato la maji katika kaunti hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo William Jillo amesema kampuni hiyo ya TAWASCO imepoteza pato kubwa kutokana na mbinu za kale za ukusanyaji wa ada za maji.
Akizungumza katika eneo la Hola kaunti ya Tana river, Jillo amesema mbinu hizo mpya ikiwemo ukusanyaji ada za maji kupitia kwa huduma ya simu kutasaidia kuongeza pato linalotokana na raslimali za maji katika kaunti hiyo.
Vile vile amesema kampuni hiyo inalenga kubadilisha mita za maji katika maeneo yote ya kaunti ya Tana river kwani zile za kale zina hitilafu na zimeisababishia kampuni hiyo hasara kubwa.
Wakati uo huo Kampuni hiyo amewahakikishia wakaazi wa kaunti ya Tana river kwamba inafanya kila juhudi kuhakikisha kuna ongezeko la maji ya kutosha kwa wakaazi wote wa kaunti ya Tana river.