Kampuni ya kutengeneza mafuta ya kupikia na vile vile sabuni ya ‘Pwani Oil’ imechangia kampeni ya kusafisha mikono katika Kaunti ya Kilifi kwa kutoa jumla ya kilo milioni 5.5 za sabuni kwa Serikali ya Kaunti hiyo.
Mkurugenzi mkuu wa mauzo wa kampuni hiyo Rajul Malde amesema mchango huo utasidia katika kuwahimiza Wakaazi wa Kaunti hiyo kubadili tabia zao kwa kukumbatia uoshaji mikono wa mara kwa mara.
Akizungumza katika kiwanda cha kutengeneza sabuni cha kampuni hiyo eneo la Kikambala Kaunti ya Kilifi mapema leo, Malde amesema wakati huu ambapo Kaunti hiyo ya Kilifi imeorodheshwa miongoni mwa Kaunti zinazokabiliwa na maambukizi ya virusi vya Corona kila juhudi zinapaswa kuwekezwa ili kuwanusuru wakaazi.
Wakati uo huo, kampuni hiyo imetoa mafuta ya kupikia na chakula cha thamani ya shilingi milioni 1.5 kitakachozinufaisha jumla ya familia elfu 10 katika Kaunti hiyo ya Kilifi.
Kampuni hiyo hapo awali ilipunguza gharama ya bidhaa zake ili kuwawezesha wateja wake kununua bidhaa za kampuni hiyo hasa baada ya taifa hili kukabiliwa na janga la Corona.