Story by Gabriel Mwaganjoni –
Kampuni ya vifaa vya kielektrokini ya LG inalenga kufungua matawi matano zaidi nchini ili kufanikisha mchakato wake wa kibiashara na kuwahudumia wateja.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo kanda ya Afrika Mashariki Sa Nyuong Kim amesema mbali na kuiweka kampuni hiyo kileleni katika biashara vile vile itapeleka huduma karibu na wateja wake mashinani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa kuwapatia huduma maalum wateja wake hadi majumbani mwao katika hafla iliyofanyika jijini Nairobi, Kim amesema maduka hayo matano maalum yatafunguliwa katika miji ya Bungoma, Kisii, Nyeri, Naivasha na Malindi katika kaunti ya Kilifi.
Kim amesema wateja wa bidhaa za LG zikiwemo runinga, majokovu, meko inayotumia gesi, viyoyozi radio miongoni mwa bidhaa nyinginezo watakuwa na uwezo wa hadi siku 7 kurudisha bidhaa endapo itakuwa na hitilafu na kubadilishiwa nyingine.
Hata hivyo mteja atakuwa na uwezo wa miaka miwili kubadilishiwa bidhaa endapo itakumbwa na hitalifu na kipindi cha miaka 10 ambapo mteja atanufaika na huduma za ukaguzi wa bidhaa zake bure majumbani.
Wakati uo huo ameongeza kwamba kampuni hiyo vile vile itaboresha huduma zake kwa wateja wake kwa kufungua karakana maalum za LG katika mataifa ya Tanzania, Ethiopia, Sudan na Kenya.