Serikali ya kaunti ya Mombasa imesitisha shughuli za kampuni moja inayoshughulika na uhifadhi wa bidhaa zinazotumiwa kutengeneza saruji huko Mikindani hadi pale mikakati yote ya kimazingira itakapozingatiwa na kampuni hiyo.
Akizungumza na wanahabari Katibu wa serikali ya kaunti ya Mombasa Francis Thoya, amesema kuwa shughuli za kampuni hiyo zimesababisha madhara ya kiafya kwa wakaazi wa eneo hilo.
Thoya amesema kwamba kampuni hiyo haiwezi kuendeleza shughuli zake huku wakaazi wakizidi kuhangaika kutokana na vumbi kali linalotokana na shughuli katika bohari hilo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadi ya Mikindani Kaunti ya Mombasa Juma Renson Thoya amesisitiza umuhimu wa wamiliki wa kampuni katika eneo hilo kuzingatia afya ya wakaazi na mazingira kabla ya kuidhinisha miradi yao ya kibiashara.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.