
Mwakilishi wa kike kaunti ya Tanariver, Rehema Hassan akihutubia wananchi mjini Hola./ Picha : Charo Banda
Wadau mbali mbali wa kupambana na ukeketaji katika kaunti ya Tanariver sasa wameshirikiana na viongozi wa eneo hilo pamoja na polisi ili kuendeleza kampeni kupitia michezo ili kukomesha ukeketaji miongoni mwa jamii za wakazi wa eneo hilo .
Akizungumza katika hafla ya kuendeleza kampeni hizo katika uwanja wa shule ya wavulana ya HOLA mwakilishi wa kike kaunti ya Tanariver Rehema Hassan sasa amefichua kuwa tangu vita dhidi ya ukeketaji kuanzishwa visa hivyo vimeanza kupungua kutoka asilimia 100 hadi 60 pekee.
Mwakilishi huyo amesema kuwa wameamua kuwashirikisha maafisa wa polisi katika kampeni hizo za kumaliza ukeketaji pamoja na mashirika mbali mbali ili kumaliza kabisa visa hivyo.
Kwa upande wake mwanaharakati wa kupambana na visa hivyo Sadia Hussein pamoja na Kassim Maende ambaye ni afisa wa polisi kwa kauli moja wamesema kuwa jamii inafaa kusitisha mila hizo zilizopitwa na wakati wakisema kuwa sasa ni wakati wa wanaondeleza ukeketaji kukabiliwa kisheria.