Waziri wa Fedha nchini Henry Rotich amekosolewa vikali kwa kuidhinisha utekelezwaji wa ushuru wa asilimia 16 kwa bei za mafuta nchini hali inayochangia kupanda kwa gharama ya maisha.
Mbunge wa Rabai William Kamoti amesema Rotich ameenda kinyume na kauli ya wabunge na Wakenya na kuchangia ugumu wa maisha, akisema Rotich anafaa kufahamu kuwa jukumu lake ni kuwahudumia wakenya na wala sio serikali.
Kamoti amelitetea bunge la kitaifa, akisema liliwajibikia kikamilifu swala la ushuru wa asilimia 16 na kamwe hawatalegeza kamba kuhusu swala hilo hadi pale mkenya atakapoondolewa mzigo huo.
Mbunge huyo wa Rabai amesema wakenya kote nchini wamechoshwa na mzigo wa gharama ya bei ya vyakula, nauli miongoni mwa gharama nyingine za maisha kutokana na mzigo wa ushuru unaoongezwa kila uchao na Serikali kuu.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.