Story by Our Correspondents-
Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameongoza wafuasi wa chama hicho na kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi, wakitaka Sonko aruhusiwe kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa.
Akizungumza na Wanahabari nje ya majengo ya Mahakama hiyo, Kalonzo amesema ni lazima haki ya wakaazi wa Mombasa izingatiwe huku akidai kwamba Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anadanganywa na maafisa wake.
Kalonzo amesema chama cha Wiper kitahakikisha kinapigania haki ya wakaazi wa kaunti ya Mombasa huku akisema kuna watu walikuwa na kesi katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC na waliruhusiwa kuwania urais wa taifa hili hivyo basi Sonko pia ana haki ya kuwania ugavana wa Mombasa.
Kesi hiyo hata hivyo imeahirishwa hadi hapo kesho mwendo wa saa tano asubuhi baada ya Tume ya IEBC kukosa kuwasilisha stakabadhi za kuonyesha sababu zilizochangia Sonko kukosa kuidhinishwa kuwania ugavana wa Mombasa.