Jumla ya watu 21 katika Kaunti ya Tana river wamepitia mateso, wakipotezwa na wengine wakiuwawa katika mchakato wa kukabiliana na ugaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utetezi wa haki za kibinadamu nchini la MUHURI Hassan Abdille japo amesema kwamba Shirika hilo linaunga mkono kikamilifu jitihada za kuudhibiti ugaidi na itikadi kali hapa Pwani, ni vyema iwapo idara ya usalama itawaandama wahusika.
Abdille amefichua kwamba kati ya mwaka uliyopita na mwaka huu, jumla ya watu 16 katika Kaunti hiyo wamepotezwa na kamwe hawajapatikana tena, watatu wameuwawa katika hali tata huku wengine wawili wakipotezwa na kisha kuteswa mikononi mwa watu wanaoaminika kuwa Maafisa wa usalama.
Mkurugezi huyo wa Shirika la MUHURI nchini hata hivyo ameitaka Serikali kuu kutumia mbinu mbadala katika kulidhibiti swala la itikadi kali hapa Pwani na kuwajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo Watetezi wa haki za binadamu katika kulikomesha tatizo hilo kuliko kutumia nguvu kupita kiasi.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.