Story Hussein Mdune-
Waziri wa Barabara na kazi za umma kaunti ya Kwale Ali Mwachiribi Joto amesema kuchelewa kwa mgao wa fedha za mwaka 2020/2021 kutoka kwa Bodi ya kitaifa ya maswala ya Barabara ndicho chanzo cha miradi mingi ya barabara kutoendelea kaunti ya Kwale.
Katika kikao na Wanahabari, Joto amesema mwaka huo hawajapokea fedha ambazo walikuwa wanapania kuendeleza miradi iliyokuwa imebuniwa kwenye wadi mbali mbali za kaunti hiyo hatua iliyochangia kukwamisha miradi hiyo.
Hata hivyo amesema wako na imani ya kuendeleza miradi ambayo ilikuwa imekwama baada ya Bodi hiyo kukubali ombi la mgao wa fedha.
Wakati huo huo amesema tayari wizara yake inaendeleza ujenzi wa kurekebisha Barabara kwenye wadi mbalimbali kaunti ya Kwale.