Katika juhudi za kuhakikisha sanaa ya humu nchini inapigia upato maadili na mambo yanayokubalika katika jamii, sasa jopokazi maalum lililobuniwa hivi majuzi limehimizwa kuisafisha sekta ya sanaa na burudani humu nchini.
Afisa mkuu mtendaji wa Bodi ya filamu nchini Dkt Ezekiel Mutua amesema hali hiyo imeafikiwa kufuatia kutikisika kwa sekta ya sanaa nchini na ambayo imezongwa na mambo machafu na ukosefu wa maadili.
Mutua amelitaka jopokazi hilo linaloshirikiana na bodi ya filamu nchini litafanya kazi na wadau wote husika mashinani ili kukuza sekta hiyo katika maadili.
Wakati uo huo amewataka wasanii kukoma kueneza matusi kupitia sanaa hasa katika mitandao ya kijamii, akisema hali hiyo inawapotosha kimaadili watoto.