Jeshi la Marekani limethibitisha kwamba afisa mmoja wa jeshi la Marekani na wahudumu wengine wawili katika kambi ya kijeshi ya Manda Kaunti ya Lamu walifariki wakati wa shambulizi la kigaidi lilitekelezwa hapo jana katika kambi hio.
Katika taarifa kutoka kwa jeshi hilo, wanajeshi wegine wawili wa Marekani walijeruhiwa vibaya japo wanaendelea na tiba ya dharura na watasafirishwa hadi marekani kwa matibabu maalum.
Kamanda mkuu wa jeshi la Marekani anayesimamia kikosi maalum Barani Afrika Stephen Townsend amesema majina ya watatu hao hayawezi kufichuliwa kwa sasa kwani jamaa zao hawajafahamishwa kuhusu maafa hayo.
Townsend amesema marekani haitawalegezea kamba wanamgambo wa Al-shabab ambao wameonekana kuimarisha mashambulizi yao katika vituo mbalimbali vya wanajeshi wa Marekani Barani Afrika.
Kauli ya Townsend inajiri huku wanajeshi wa Marekani wakiwatia nguvuni washukiwa wa Al-shabab waliyojaribu kuingia kwa lazima katika kambi ya wanajeshi wa marekani eneo la Nanyuki Kaunti ya Laikipia mapema leo.