Baada ya mgogoro wa zaidi ya miezi mitatu kati ya Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Granton Samboja na Wajumbe wa bunge la Kaunti hiyo, sasa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ameingilia kati ili kuutanzua utata huo.
Joho aliyekutana na Wajumbe wote wa bunge la Kaunti hiyo sambamba na Spika wao, Meshack Maganga na Mbunge wa Taveta, Dakta Naomi Shaban amesema atakutana na Samboja ili kusawazisha utata huo na kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza majukumu yao mara moja kwa wakaazi wa Kaunti hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi aliyehudhuria mkao huo uliyofanyika mjini Mombasa hii leo ameshikilia kwamba ni muhimu viongozi hao waafikiane kwani mgogoro huo umelemaza mchakato wa kimaendeleo katika Kaunti ya Taita Taveta.
Akizungumza katika mkao huo, Mbunge wa Taveta Dakta Naomi Shaban amewaomba msamaha wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta kufuatia utata huo akisema mgogoro huo utatanzuliwa hivi karibuni na viongozi wote kutekeleza majukumu yao kikatiba.
Kauli ya Bi Shaban imeungwa mkono kikamilifu na Spika wa bunge la kaunti ya Taita Taveta, Meshack Maganga huku akisema kuwa kila jitihada zimewekezwa ili kuutanzua mgogoro huo na kufanikisha huduma msingi kwa wakaazi wa Kaunti hiyo.