Story by Gabriel Mwaganjoni-
Jamii ya kaunti ya Mombasa imehimizwa kuwa wazi na kushiriki vita dhidi ya uhalifu katika kaunti hiyo.
Hii inafuatia msururu wa visa vya uhalifu na mauaji hasa katika gatuzi dogo la Kisauni siku mbili zilizopita.
Seneta maalum Miraj Abdilahi amesema pindi jamii itakaposimama kidete na kuwafichua wahalifu miongoni mwao basi swala la utovu wa usalama katika kaunti hiyo litatatuliwa.
Kiongozi huyo ameisihi jamii ikome kuchukua sheria mikononi akisema hali ya kulipiza kisasi na kuwateketeza washukiwa wa uhalifu itapelekea watu wengine wasiokuwa na hatia kuuwawa kinyama.
Hata hivyo amehoji kwamba ni sharti wadau wote husika waungane katika kuzima misururu ya visa vya uhalifu hasa katika maeneo ya Kisauni na Likoni ambayo yamekuwa yakishuhudia hali tata ya kiusalama.
Kauli ya Miraj inajiri baada ya jumla ya watu 5 kuuwawa ndani ya kipindi cha siku mbili tu katika gatuzi dogo la Kisauni kufuatia misururu ya visa vya uvamizi wa magenge ya kihalifu katika eneo la Junda.