Story by: Gabriel Mwaganjoni
Jamii katika kaunti ya Mombasa inakashfiwa kwa kubuni soko la bidhaa mbalimbali za wizi, hali ambayo imechangia kuendelea kwa visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.
Kulingana na Shirika la vijana la Kadzandani Creative, kupitia kwa Mkurugenzi wake mkuu Omar Chai, wazazi wamekuwa wakifurahikia simu za rununu na bidhaa nyingine za wizi kutoka kwa watoto wao wanaofahamu vyema kwamba kamwe hawana ajira ya kununua bidhaa hizo za thamani.
Akizungumza katika mtaa wa Kadzandani gatuzi dogo la Nyali kaunti ya Mombasa katika kikao cha vijana kilichopania kulijadili swala la usalama eneo hilo, Chai amesema maeneo ya Nyali na Kisauni yameathirika na hali hiyo ndiposa wanaharakati hao wa vijana wameungana ili kuupiga vita uhalifu.
Mwanaharakati huyo wa Vijana aidha amesema baada ya vikao hivyo vya vijana vile vile watawahusisha wazazi katika maeneo hayo ya Kisauni na Nyali ili kujadili jinsi ya kudhibiti uhalifu unaowahusisha vijana wadogo mno katika maeneo hayo.