Picha kwa hisani –
Maafisa wa polisi katika eneo la Likoni kaunti ya Mombasa wameimarisha msako wao dhidi ya genge la majambazi ambalo limekuwa likiwahangaisha wakaazi wa maeneo ya Shika Adabu katika eneo hilo.
Hii ni baada ya mshukiwa mmoja wa ujambazi kupigwa risasi na kuuwawa usiku wa kuamkia leo.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Jane Munywoki amesema Matano Masoud mwenye umri wa miaka 22 amepigwa risasi na Maafisa wa polisi katika eneo la Kona ya zamani huko Likoni huku wenzake wakitoroka mtego wa polisi.
Munywoki amesema genge hilo limekuwa likiwaibia wakaazi na hata kuwauwa kwa kuwadunga visu au kuwakata kwa mapanga watu wasiokuwa na hatia akiapa kulizima genge hilo.
Mwili wa marehemu umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani huku oparesheni kali ya kiusalama ikiimarishwa katika Gatuzi zima dogo la Likoni.