Story by Our Correspondents
Jaji mkuu nchini Martha Koome amesema hatua yake ya hivi majuzi ya kufanya kikao na rais William Ruto haijakandamiza uhuru wa Idara ya Mahakama nchini.
Jaji Koome amesema kufanya mazungumzo na mihimili mengine ya serikali ili kutatua changamoto katika usimamizi wa haki, hakuwezi hujumu uhuru wa idara ya Mahakama, hususan iwapo wahusika hawatojadili jinsi Mahakama inavyopaswa kutoa uamuzi wa kesi zinazowasilishwa.
Akizungumza wakati wa mkutano uliowaleta pamoja wakuu wa Mahakama ili kujadili utendakazi na uhuru wa idara hiyo, Jaji Koome ameeleza haja ya kutathmini jinsi Mahakama inavyoshughulikia kesi zinazoathiri sera na maslahi ya umma.
Aidha amesema yanayopaswa kaungaziwa zaidi ni masuala yanayohusu muda wa kusikiliza na kuamua kesi zinazohusisha miradi ya serikali inayopaswa kutekelezwa kwa wakati maalum, akisema kuweka tarehe ya mbali ya kusikiliza kesi hizo inaathiri utekelezwaji wa miradi hiyo.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 22 mwezi uliopita wa Januari, Koome alifanya mazungumzo na rais Ruto pamoja na uongozi wa bunge kuangazia suala la ufisadi katika Idara ya Mahakama, ambapo baadhi ya wakenya wakiongozwa na mrengo wa upinzani walikosoa vikali kikao hicho.