Story na Janet Shume –
Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu haki na sheria imemhoji Jaji mkuu mteule Martha Koome kuhusiana na uwajibikaji wake iwapo bunge la kitaifa litamuidhinisha kuwa Jaji mkuu nchini.
Akiwa mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kangema Muturi Kigano, Jaji Koome ameelezea ufanisi wake wa kikazi, akisema tajriba yake ya uanasheria unampa uwezo wa kukakikisha idara ya Mahakama nchini inatekeleza majukumu yake.
Jaji Koome amesema maono yake katika idara ya Mahakama ni kuhakikisha huduma katika idara hiyo zinaimarika pakubwa ili kuwahudumia wakenya kwa haki na kweli huku akisema kuna haja ya uongozi wa serikali, mabunge yote mawili kushirikiana na idara ya mahakama ili kuimarisha huduma za mahakama.
Akijibu swali la migogoro ya ardhi inayoshuhudiwa humu nchini hasa kaunti za Pwani lililoulizwa na Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kwale Zuleikha Hassan, Jaji Koome amesema atahakikisha idara ya Mahakama inashirikiana na serikali za kaunti na bunge ka kitaifa ili kuleta huduma za mahakama karibu na mwananchi.
Akigusia swala la ufisadi nchini, Jaji Koome amesema japo swala la ufisadi limekuwa donda sugu atahakikisha anaweka mikakati muafaka ya kulinda mali ya umma na wafisadi wanaadhibiwa.