Story by Our Correspondents-
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imetangaza rasmi tarehe ya uchaguzi mdogo wa useneta katika kaunti ya Bungoma ambao utaandaliwa tarehe 8 mwezi Disemba mwaka huu.
Tangazo hilo ambalo limechapishwa katika gazeti rasmi la Serikali, limejiri baada ya aliyekuwa Seneta wa kaunti hiyo Moses Wetangula kuchaguliwa kuwa Spika wa bunge la kitaifa majuma mawili yaliopita.
Katika tangazo hilo lililotiwa saini na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, maeneo mengine ambayo yataandaliwa uchaguzi huo ni pamoja na wadi ya Ololmasani, Kyome/Thaana, Utawala, Mumis Kazkazini, Nairobi mjini, Kakamega na baadhi ya maeneo ya kaunti ya Siaya.
IEBC imepeana muda wa hadi tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka huu kwa vyama vya kisiasa kuhakikisha vinawasilisha majina ya wagombea wao ili kurahisisha zoezi hilo la uchaguzi mdogo huku kampeni za uchaguzi huo zikiratibiwa kuanza tarehe 9 mwezi Novemba hadi tarehe 6 Disemba mwaka huu kabla ya siku ya uchaguzi huo.