Story by Mimuh Mohamed-
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imefanya kikao maalum na Wanahabari na wadau wengine husika kujadili mikakati itakayofanikisha uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022.
Akizunguma katika kikao hicho mjini Mombasa, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema tume hiyo inahitaji shilingi bilioni 40.9 ili kufanikisha uchaguzi mkuu ujao bila changamoto.
Chebukati amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 40.3 zitatumika kununua vifaa vya uchaguzi huku shilingi milioni 588 zikipangiwa ununuzi wa vifaa vya kudhibiti maambukizi ya Corona wakati wa uchaguzi ikiwemo vieuzi na sabuni.
Chebukati aidha amesema tume ya IEBC haitoidhinisha orodha za wabunge na maseneta wateule wa vyama vya kisiasa iwapo uteuzi huo hautazingatia sheria ya tuluthi mbili ya usawa wa jinsia kama ilivyoagiza Mahakama kuu.
Mwenyekiti huyo wa IEBC amesema tume hiYo inashirikiana na vitengo vyengine husika kuhakikisha unyanyasaji wa maafisa wa uchaguzi na Wanahabari haushuhudiwi wakati wa uchaguzi mkuu kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2017.
IEBC aidha imesema uchaguzi mkuu ujao utaandaliwa rasmi tarehe 9 mwezi Agosti mwaka wa 2022.