Story by Our Correspondents –
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imesema tangu zoezi la usajili wa wapiga kura kuzinduliwa rasmi humu nchini kwa kipindi cha siku 30, idadi ya watu iliyojitokeza kusajiliwa ni ndogo mno.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, IEBC imedai kufaulu kuwasajili wapiga kura elfu 200 pekee kufikia sasa licha ya Tume hiyo kulenga kuwasajili watu milioni 1.5 kila wiki.
Tume hiyo ambayo inalenga kuwasajili wapiga kura milioni 6 kabla ya zoezi hilo kukamilika Oktoba 30, imesema ni kaunti za Wajir, Pokot Magharibi, Mandera, Samburu, Elgeyo Marekwet, Baringo, Nandi, Narok, Turkana na Tanariver ambazo zimeandikisha idadi ya juu ya wanaojisajili.
Hata hivyo kaunti za Mombasa, Nairobi, Embu, Laikipia, Kitui, Murang’a, Nyandarua, Kiambu, Kirinyaga na Nyeri zimesajili idadi ndogo ya wapiga kura.
Wakati uo huo Tume hiyo imewahimiza wananchi kutopuuza zoezi hilo na badala yake kujitokeza na kujisajili kama wapiga kura ili kuafikia idadi inayohitaji na Tume hiyo kabla ya uchaguzi mkuu ujao.