Story by Mimuh Mohamed –
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imekutana na maafisa wa vitengo mbali mbali vya serikali ikiwemo wa idara ya mahakama, usalama na wadau wengine husika kujadili mikakati kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wanahabari baada ya kukamilika kikao hicho cha faragha, Jaji mkuu nchini Martha Koome amesema maafisa wa vitengo hivyo watakutana mara kwa mara kutathmini utayari wa vitengo hivyo na kusimamia uchaguzi huru na haki.
Bi Koome aidha amesema idara ya mahakama iko tayari kushuhulikia kesi zote zitakazowasilishwa mahakamani kuhusiana na uchaguzi ujao,akitoa muda wa siku 90 kwa maafisa wa idara ya mahakama kusikiza na kuamua kesi zote za uchaguzi zilizowasilishwa awali na ambazo hadi sasa hazijashughulikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema tangu kuanza kwa zoezi la usajili wa wapiga kura kufikia sasa tume hiyo imefanikiwa kusajili takriban wapiga kura elfu 760, akitoa hakikisha kwamba tume hiyo itazidisha ushirikiano na vitengo muhimu vya serikali kuhakikisha wanaandaa uchaguzi huru na haki.
Naye Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i amesema idara ya usalama itashirikiana kikamilifu na IEBC kufanikisha uchaguzi wa amani huku akisema wataongeza maafisa wa polisi watakaosimamia uchaguzi ujao.