Story by Hussein Mdune-
Baadhi ya viongozi wa kidini kaunti ya Mombasa wamedai kutoridhishwa na mvutano unaoshuhudiwa kati ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC na idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI kuhusu uchaguzi.
Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Ushindi Baptism eneo la Likoni Joseph Maisha, viongozi hao wamesema mvutano huo huenda ukasababisha ukosefu wa amani wakati huu ambapo taifa linajiandaa na uchaguzi mkuu.
Askofu Maisha amezitaka taasisi hizo mbili kusitisha mara moja malumbano hayo na badala yake kila taasisi kuwajibikia majukumu yaake kwa mujibu wa katiba.
Wakati huo uo ameitaka idara ya usalama nchini kuweka ulinzi wa kutosha katika maeneo ya mipakani ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Agosti 9 unashuhudia amani.